ISRAEL:MATOKEO YA AWALI YA UCHAGUZI HALI TETE
Benjamin Netanyahu akabiliwa na hali ngumu
Ripoti za
matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Israel zinaonyesha waziri mkuu
Benjamin Netanyahu ameendelea kukabana koo na mpinzani wake mkubwa Benny
Grantz.
Vyombo mbalimbali vya
habari vya Israel vimeripoti kwamba chama cha Netanyahu cha mrengo wa kulia cha Likud
na kile cha Bluu na Nyeupe cha mpinzani wake Grantz kila kimoja kimepata viti
32 kati ya viti 120 vya bunge baada ya takriban asilimia 90 ya kura
kuhesabiwa.
Ripoti hizo
zilinukuu duru kutoka tume ya uchaguzi kwani kiwango hicho cha matokeo
kilikuwa hakijachapishwa rasmi na hakikutarajiwa kabla ya leo alasiri.
Matokeo ya
awali katika uchaguzi wa Israel kwa kawaida huwa si ya uhakika na huku matokeo
rasmi yakitarajiwa kutolewa Jumatano, huenda bado Netanyahu akapata ushindi,
ingawa vituo vyote vitatu vimeonyesha matokeo sawa.
Kwa matokeo
hayo, pande zote zitatakiwa kuunda serikali itakayojumuisha vyama vingine
bungeni hali inayoibua uwezekano wa mazungumzo kuelekea kuundwa kwa
serikai ya umoja.
Iwapo matokeo haya ya
awali yatabakia hivyo hadi mwisho, itakuwa ni pigo kubwa kwa Netanyahu,
aliyekuwa na matarajio ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vya mrengo wa
kulia, sawasawa na ule uliopo sasa, huku pia akikabiliwa na uwezekano wa
kufunguliwa mashitaka ya ufisadi wiki chache zijazo.
Kwenye
mkutano na wafuasi wa chama chake baada ya uchaguzi mjini Tel Aviv jana usiku
Netanyahu aliashiria kwamba tayari amejiandaa kwa makubaliano magumu ya kuunda
serikali ijayo ya muungano ya Israel, huku akisisitiza umuhimu wa Israel kuwa
na serikali imara itakayoutetea kwa nguvu zote Uyahudi.
Amesema,
bado anasubiri matokeo rasmi, lakini akisisitiza kwamba Israel iko njia panda
kihistoria lakini pia ikiwa na fursa pana pamoja na changamoto kubwa katika
siku za usoni, huku akigusia alivyoviita ''vitisho halisi'' kutoka kwa Iran na
washirika wake, "Siku chache zijazo mpango wa karne utawasilishwa kwa
rafiki yangu wa karibu rais Trump na makubaliano yatakayofuata yatatengeneza
mustakabali wa taifa letu kwa ajili ya kizazi kijacho. Kwa wakati huu, Israel
inahitaji serikali thabiti, imara na ya Kiyahudi ili kufikia malengo
hayo."
Dalili zote
zinaonyesha kuwa hakuna anayeweza kupata idadi kubwa ya wabunge kati ya
Netanyahu na Gantz bila uungaji mkono wa Avigdor Lieberman aliyekuwa waziri wa
ulinzi wa Netanyahu. Lieberman ameibuka kama mshindi wa kweli, kwani kuna
uwezekano mkubwa kwamba ndiye atakayeamua juu ya atakayejumuishwa katika
serikali ijayo. Chama chake cha Yisrael Beitenu kimepata viti tisa.
Wabunge
katika chama cha Gantz pia wameelezea uungaji mkono wao wa serikali ya muungano
ambayo huenda ikajumuisha wadhifa wa waziri mkuu ambao utakuwa unazunguka kwa
watu tofauti.
Baaada ya
matokeo hayo ya awali, Lieberman alitoa mwito wa serikali ya muungano wa chama
chake, Likud na Bluu na Nyeupe akisema taifa hilo linakabiliwa na hali ya kile
alichotaja kuwa ni "dharura."
Huu ni
uchaguzi wa pili katika kipindi cha miezi mitano nchini humo na rais Reuven
Rivlin ambaye anatakiwa kuchagua mtu wa kuunda serikali ijayo akisema, ni
lazima wajizuie kufanya uchaguzi mwingine.
Wagombea watatu wnaoshikana mashati kwenye uchaguzi wa Israel. Kutoka kushoto Beny Gantz, Avigdor Lieberman na Benjamin Netanyahu.
Comments
Post a Comment