MAGUFULI;JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI LILITELEKEZWA
Rais John Magufuli aahidi kutekeleza miradi ya maji Singida Mashariki
Tundu Lissu, kutoka chama cha upinzani cha Chadema alichaguliwa
kuliongoza jimbo hilo kwa mara ya pili 2015, lakini toka Septemba 7, 2017
amekuwa nje ya Tanzania kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu
wasiojulikana.
Katika kipindi chote hicho, jimbo hilo limekuwa wazi bila ya
mwakilishi bungeni.
"Saa nyengine majimbo yanakosa uwakilishi...Kama
ulivyoagiza mheshimiwa Spika (Job Ndugai) kwamba tushughulikie tatizo la maji
katika jimbo lile…kama tulivyoshughulikia jimbo la Dar es Salaam…ninakuahidi
kwamba serikali yangu itashughulikia, ili yale yaliyokuwa yamechelewa yaanze kufika
haraka haraka," amesema Magufuli.
Mwezi Juni mwaka huu alifutwa ubunge rasmi na Spika Job Ndugai
amabaye alitaja sababu kuu mbili za kufanya uamuzi huo. Sababu ya kwanza
ilotajwa ni utoro bungeni na ya pili ni kutojaza fomu za mali na madeni.
Baada ya kuvuliwa ubunge kwa Lissu, Miraji Mtaturu kutoka chama
cha CCM akapita bila kupingwa.
Hii leo amesifiwa na Rais Magufuli kwa kuanza kazi kwa kasi.
Magufuli ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa rada za
kuongozea ndege za kiraia nchini Tanzania.
Mtaturu yupo kwenye kamati ya miundombinu ya bunge na alikuwepo
kwenye uzinduzi wa rada.
"Tanzania haizuiliki"
Serikali ya Tanzania inatekeleza mradi wa ujenzi wa rada nne,
kati ya hizo mbili, ya Dar es Salaam na Kilimanjaro zimekamilika na kuzinduliwa
leo.
Ujenzi bado unaendelea katika mikoa ya Mwanza na Songwe. Jumla
mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.3.
Kabla ya ujenzi huo, Tanzania ilikuwa na uwezo wa kufuatilia
safari za ndege kwenye eneo la asilimia 25 tu ya anga lake.
Hali hiyo ilikuwa ikiipatia Kenya wastani wa shilingi za
Tanzania bilioni moja kwa kuongoza ndege kwenye anga la Tanzania.
Baada ya uzinduzi wa rada hizo mbilisasa Tanzania itakuwa na
uwezo wa kuongoza ndege kwa asilimia 75 ya anga lake.
Katika uzinduzi huo Rais Magufuli amesema juhudi za serikali
yake katika kuendeleza sekta ya anga hazizuiliki.
Amesema wote wanaojaribu kubeza ama kuzuia Shirika la Ndege la
Nchi hiyo (ATCL) hawatafika popote na kudai wanayoyafanya ni sawa na
"kelele za chura."
"Mkiona watu wanakamata ndege yetu msishangae. Kwa sabubu
shirika letu linafanya vizuri."
Magufuli pia amejaribu kutumia mashairi ya kibao cha
Extravaganza cha bendi ya Suti Sol ya Kenya: "...wakifunika,
tunafungua...hawazuiliwa kufanya kitu. Wakiwafungia kuingia ndani, wanawakuta
wapo ndani. Sasa sisi ni hivyo hivyo. Wajijaribu hivi, tutafanya hivi.
Wakifanya hivi tutafanya hivi.Ili nchi yetu iendelee mpaka ifike
tunapopanga."
Comments
Post a Comment