RWANDA AND UGANDA KUFIKIA MAKUBALIANO KUBORESHA USALAMA
Wajumbe wa serikali za Rwanda na Uganda ambao wamekutana mjini
Kigali Jumatatu, wamekubaliana mambo kadha ikiwemo kujiepusha na harakati za
kuyumbisha usalama katika nchi mojawapo.
Katika taarifa ya pamoja iliyokamilisha kikao hicho, Rwanda
imetoa orodha ya raia wake wanaozuiliwa nchini Uganda, na serikali ya Uganda
imekubali kuchunguza kwa kina taarifa hiyo, na kuhakikisha wale ambao watakutwa
hawana hatia kuachiliwa huru.
Pande hizo zimekubaliana pia kusahihisha mkataba wa kuwarudisha
makwao watuhumiwa wa uhalifu. Wajumbe kwenye mkutano huo wa mjini Kigali
wamekubaliana na kuachana na tabia ya kutumia vyombo vya habari au mitandao ya
kijamii, kwa kufanya propaganda ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa nchi zao.
Aidha pande zote zimesema suala la uhuru wa usafiri wa watu na
vitu kwenye mpaka wa nchi zao, litajadiliwa katika kikao kingine ambacho
kitafanyika mjini Kampala, baada ya kipindi cha siku 30.
Ujumbe wa Uganda kwenye mkutano huo wa Kigali ulikuwa unaongozwa
na waziri wa mambo ya nje, Sam Kutesa, nao ujumbe wa serikali ya Rwanda ulikuwa
unaongozwa na waziri wa mashauri ya kigeni Olivier Nduhungirehe.
Waziri wa Mambo ya nje wa Angola Manuel Domingos Augusto, na
naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, pia Waziri wa Mambo
ya Ndani na Usalama Gilbert Kankonde Malamba, walishiriki kwenye mkutano huo
kama wawakilishi wa wasuluhishi ambao ni marais wa Angola na DRC.
Walipokutana mjini Luanda, Angola, mwezi uliopita, marais Paul
Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda walikubaliana kumaliza mzozo wa
kisiasa kati ya nchi zao kupitia mazungumzo.
Comments
Post a Comment