KILIMO BORA CHA VITUNGUU MAJI NA SOKO LAKE





UTANGULIZI
Vitunguu maji kwa kitaalamu hujulikana kama Allium cepana kwa kiingereza huitwa Bulb Onions. Vitunguu ni zao muhimu sana sio kwa matumizi ya ndani tu lakini pia ni zao la kibiashara linaloweza kukuletea kipato kikubwa. Vitunguu ni zao la bustani ambalo lipo kwenye kundi la mboga (vegetables).

Zao hili ni maarufu kutokana na thamani ya virutubisho ilivyonavyo na ladha yake kwenye mapishi ya vyakula mbalimbali. Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima. Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini.

Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k Nchini mwetu vitunguu hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Tanga,  Arusha sehemu za Mang’ora na Babati, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Iringa wilaya ya Kilolo mpakani mwa mkoa wa Morogoro na kwenye maeneo ya mto Ruaha , Mara , Morogoro wilayani Kilosa sehemu za Lumuma na Malolo ,Mbeya Kilimanjaro na baadhi ya sehemu za Mkoa wa Singida.

Katika shamba lililo hudumiwa vizuri na kupandwa katika hali ya hewa na aina ya mbengu. Vitunguu hutoa kiasi cha tani (10) hadi 16 kwa ekari moja. Kilimo cha Vitunguu ni mojawepo ya vilimo vyenye  manufaa mengi kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya vitunguu kwa maisha ya mwanadamu, kiafya, kitabibu na kwa ajili ya kutengeneneza au kuchanganyia katika dawa tofauti. Pia ni kiungo mahususi katika mambo ya mapishi.  Hapo awali kitungu kilikuwa ni zao lililokuwa linapatikana porini katika ukanda wa bahari ya Mediterania.

Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi 20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).

Kitunguu hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, na pia hutumika kama dawa ya kansa ya tumbo, vidonda na majipu.

AINA ZA VITUNGUU
Vitunguu maji vimegawanyika katika makundi matatu:
KUNDI LA KWANZA: VITUNGUU VYEUPE (WHITE ONIONS).  Vitunguu hivi ni vyeupe nje na nadni pia: Mfano ni White granex, snow white

KUNDILA PILI: VITUNGUU VYA NJANO (YELLOW ONIONS).
Vitunguu hivi hua na rangi ya dhahabu kwa nje, ila ndani nyama yake ni ya njano mpauko.  Vitunguu hivi ni vitamu (ladha ya sukari) kuliko aina nyingine ya vitunguu. Mfano: Texas Supersweet, Walla Walla Sweet, Granex Yellow Hybrid, Candy Hybrid

KUNDI LA TATU: VITUNGUU VYEKUNDU (RED ONIONS): 
Hivi vina rangi nyekundu kwa nje na ndani kunakua na rangi nyeupe. Mfano Red Creole, Red Bombay, Neptune F1, Tajirika, Meru Super, Mang’ola Red, JAMBAR F1, n.k Aina hizi za vitunguu vyekundu ndizo hupendwa zaidi na walaji na ndio huzalishwa kwa wingi. Hivyo katika mafunzo yetu tutajikita zaidi kwenye aina hizi za vitunguu vyekundu.

AINA ZA MBEGU ZA VITUNGUU
Kuna aina tatu za mbegu za vitunguu.AINA YA KWANZA: MBEGU ZA KIENYEJI:   Hizi ni zile mbegu zinazozalishwa na wakulima wenyewe. Mara nyingi mbegu hizi zinakua hazijathibitishwa na wataalamu kutoka taasisi ya kuthibiti ubora wa mbegu (TOSCI). Wakulima wanazalisha mbegu hizi na kuwauzia wakulima wengine kwa kutumia kipimo cha kilo au debe.

Wakulima wengi hupendelea mbegu hizi za kienyeji kwa vile bei yake ni ndogo. Mbegu hizi maeneo mengi huuzwa kati ya 20,000 hadi 30,000 kwa Kilo moja ya mebgu.Kutokana na kwamba mbegu hizi zina ubora mdogo, mkulima inambidi atumie mbegu nyingi ili kutosheleza mahitaji ya ekari moja.

Kwa ekari moja mkulima hutumia kilo 6 hadi 10 za mbegu hizi ili kutosheleza. Kama mtaalamu wa kilimo simshauri mkulima anayetaka kulima kibiashara kutumia mbegu hizi za kienyeji kwa maana hata Mavuno yake hayatabiriki. Ila Sio kwamba mbegu zote zinazozalishwa na wakulima ni mbaya, hapana.

Upo utaratibu wa wakulima kuzalisha mbegu kitaalamu kwa kufuata utaratibu ulipo kisheria. Mbegu hizo zinazozalishwa na wakulima kitaalamu huitwa mbegu za daraja la kuazimiwa (quality declared seeds) au kwa kifupi huitwa QDS. Mbegu hizi za QDS zina mipaka yake ya eneo la kutumika.

Na wazalishaji wa QDS lazima wapate mafunzo na wasajiliwe na Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (Tanzania Official Seed Certification Institute) au kwa kifupi TOSCI. TOSCI pia wana utaratibu wa kufanya ukaguzi na kutoa kibali cha mbegu hizo za QDS kuuzwa kama zimekizi vigezo husika. Kama hazijakizi mbegu hizo haziruhusiwi kuuzwa kwa wakulima.

AINA YA PILI: MBEGU ZA KAWAIDA (OPEN POLLINATED VARIETIES)  au kwa kifupi huitwa OPV. Mbegu hizi zimezalishwa kitaalamu kwa njia ya Uchavushaji ya wazi (Open Pollination). Mbegu hizi ndio zinazouzwa kwa wingi na makampuni ya mbegu.Bei yake ni kati ya 60,000 hadi 100,000 kwa kilo. Hii inategemeana na kampuni na aina ya mbegu. Mbegu hizi kwa ekari moja utatumia Kilo 3 hadi 4. Mfano wa mbegu za OPV ni: Bombay Red, Red Creole, Tajirika, Meru Super n.k.

AINA YA TATU: MBEGU CHOTARA (HYBRID)
 Hizi ni aina ya mbegu zinazozalishwa kitaalamu sana kuliko hizo aina nyingine nilizozitaja hapo juu. Mbegu hizi hua na sifa za kipekee, kama vile kua na mavuno mengi, kuwa na ukinzani kwa baadhi ya magonjwa, kukomaa haraka n.k. Nyingine hutengenezwa kutokana na sifa maalumu zinazohitajika na walaji au soko, kama vile rangi, ukubwa (size), harufu, ladha n.k.

Pia mbegu hizi huuzwa ghali zaidi. Bei yake ni kati ya 300,000 hadi 600,000 kwa Kilo moja. Kilo moja na nusu au Kilo 2 hutosha kwa ekari moja. Mfano wa mbegu hizi ni kama Neptune F1, RedStar F1, JAMBAR F1 n.k

AINA ZA KILIMO CHA VITUNGUU
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbiliGreen House Shambani

HALI YA HEWA NA UDONGO UFAAO KWA KILIMO CHA VITUNGUU
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.

Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu. Sehemu nyingi zinazostawi vitunguu maji hufaa pia kwa zao hili. Maeneo ya mwinuko wa kiasi cha zaidi ya mita 1000 juu ya usawa wa bahari hufaa zaidi.

KUTAYARISHA SHAMBA
Lima shamba kwa trekta, kwa ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45 Weka matuta ya mwinuko yenye upana wa mita 1 hadi mita 1.5 kutoka kati kati ya tuta na tuta na upana wa mita 1 Lainisha udongo au kwa kitaalamu inaitwa Harrowing. Yaani yale mabonge makubwa makubwa ya udongo yanagongwa na kutengneza udongo mlaini. Harrow ifanyike wiki 2 au 3 baada ya kulima.

Zipo trekta zinazofungwa mashine ya kufanya harrowing. Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Matutu au majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

UPANDAJI WA MBEGU ZA VITUNGUU
Vitunguu vinaweza kupandwa kwa njia mbili:

 NJIA YA KWANZA:  UPANDAJI WA MOJA KWA MOJA (DIRECT PLANTING).
Namna ya Kupanda vitunguu kwa njia ya moja kwa moja: Andaa shamba vizuri, udongo uwe mlaini, usiwe na mabongemabonge ya udongo. Weka  mbolea ya samadi kwa kutawanya (broadcasting) kisha ichanganye vizuri na udongo.

Mbolea ya samadi inayotosha kwa ekari moja ni tani 16. Baada ya kuchanganya vizuri samadi kwenye udongo, tengeneza mistari (drills) yenye kina cha sentimita 2.5 na yenye umbali wa sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari.

Kumbuka hii mistari ni kama mifereji midogo mwembamba ambayo itatumika kuweka mbegu. Hivyo zingatia vipimo. Weka mbolea ya kupandia kwenye hiyo mistari uliyotengeneza. Mbolea hii inapaswa kua na kirutubisho cha Phosphorous (Phosphate fertilizer). Mfano wa mbolea za kupandia ni kama DAP, MAP, TSP n.k.

Ukishanyunyizia mbolea ya kupandia ichanganye vizuri na udongo. Sia mbegu kwenye hiyo mifereji halafu funika kwa udongo. Kisha mwagilia mara kwa mara kadri mahitaji yanavyoongezeka. Hapa ina maana kwamba kadri mmea unavyokua ndivyo unahitaji maji mengi zaidi. Mimea ikashakua, punguza mimea, na uache sentimita 8 (cm) kati ya mmea na mmea. Ile mimea unayoipunguza   inaweza kupandwa sehemu nyingine.Hivyo basi nafasi ya mimea itakua ni 30 X 8 cm. Yaani mstari hadi mstari ni sentimita 30 na nafasi ya mche hadi mche ni sentimita 8.

NJIA YA PILI: UPANDIKIZAJI WA MICHE (TRANSPLANTING).
Hapa Miche inakuzwa kwenye kitalu kwa wiki 6 hadi 8 tangu kisia mbegu kisha inahamishiwa shambani. Inakadiriwa kwamba wiki 6 hadi 8 miche itakua imefikia kiwango kizuri cha ukuaji kwa ajili ya kuhamishiwa kwenye shamba kuu (main field).

Hii ndio njia inayoshauriwa zaidi na ndiyo inayotumia na wakulima wengi wa vitunguu. Hapa Tanzania upandaji wa mbegu za vitunguu katika kitalu kwa ujumla huanza mwezi machi hadi mei kutegemea na msimu wa kilimo.

Hivyo kilimo hiki hufanyika mara baada ya mvua za masika kubwa kuisha. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji mzuri wa vitunguu. Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari.

Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.

JINSI YA KUKUZA MICHE VITUNGUU KWENYE KITALU
Tengeneza matuta yaliyoinuka (raised seed beds) yenye upana wa mita 1 na urefu utakaopenda. Urefu mzuri wa tuta unaweza kuanzia mita 2 hadi 5. Idadi ya matututa itategemea na wingi wa mbegu unazotaka kusia. Weka Mbolea ya samadi iliyooza vizuri. Itawanye vizuri kwenye matuta ya kitalu Weka Mbolea ya kupandia ya viwandani kama TSP au MAP.

Kisha changanya vizuri na udongo. Hakikisha Samadi, mbolea ya ya Kupandia TSP vyote vinachanganyika vizuri kwenye udongo. Tengeneza mistari ambayo iko kama mifereji midogo yenye urefu wa sentimita 2. Mistari hiyo iwe umbali wa sentimita 5 kutoka mstari hadi mstari.Sia mbegu za vitunguu kwenye mistari hiyo kisha funika na udongo kidogo. Funika tuta lako kwa nyasi zilizokauka. Nyasi zinasaidia kutunza unyevunyevu wa udongo pamoja na joto la udongo litakalosaidia miche kuota vizuri.

Mwagilia maji mara kwa mara. Umwagiliaji unapaswa kuzingatia unyevunyevu wa udongo. Epuka kuzidisha maji kwenye kitalu maana husababisha magonjwa ya fungus (fungal diseases) kama Kinyausi (Damping Off). Ondoa Nyasi mara mimea inapoanza kuchomoza juu ya udongo.

Kama ni msimu wa jua kali, tengeneza kichanja ambacho juu yake utafunika na nyasi chache ili kupunguza ukali wa mionzi ya jua kwenye miche. Kila tuta unaweza kulijengea kichanja chake.  . Hakikisha kitalu hakina magugu wakati wote, kwa maana vitunguu vina mizizi mifupi (shallow roots) na haiwezi kushindana na magugu.Pandikiza miche yako kwenye shamba kuu mara miche inapofikia urefu wa sentimita 15.

Mara nyingi huchukua muda wa wiki 6 hadi 8 toka kusia mbegu hadi kufikia kupandikizwa. Maeneo ya joto ukuaji wa miche ni wa haraka zaidi, chini ya wiki 6 miche inakua tayari.

UPANDIKIZAJI WA VITUNGUU.
Vitunguu vinapsawa kupandikizwa wakati wa asubuhi au au jioni. Wakati wa jioni ndio mzuri zaidi wa kuhapandikiza miche. Miche inapaswa kupandwa kina kilekile kama ilivyokua kwenye kitalu. Yaani mche unapong’olewa kwenye kitalu kuna sehemu ilikua chini ya ardhi.

Kwenye kupandikiza urefu uleule uliokua chini ya ardhi wakati mche ulipokua kwenye kitalu ndio unapaswa kufunikwa na udongo wakati wa kupandikiza. Nafasi ya upandaji wa miche unapaswa kua sentimita 30 kwa 8 (30 X8 cm).

Yaani urefu wa mstari na mstari uwe sentimita 30 na nafasi ya mche na mche iwe sentimita 8. Nafasi inaweza kutoafutiana kidogo kulingana na aina ya mbegu, lakini pia kulingana na ukubwa wa kitunguu unachotaka. Ukitaka vitunguu vikubwa, nafasi inaongezeka, yaani vinapandwa mbalimbali. Ukitaka vitunguu vidogo unapunguza nafasi, yaani unapanda karibukaribu.

MATUMIZI YA MBOLEAKUNDI LA KWANZA: 

MBOLEA ZA KUPNADIA.

Hizi huwekwa kabla au mara tu ya kuhamishia miche shambani. Mbolea hizi zina lengo la kusaidia ukuaji mzuri wa mifumo ya mzizi (root systems) itakayosaidia mmea kufyonza virutubisho na maji kutoka ardhini.

Mbolea hizi zina kirutubisho kikuu cha Phosphorous, na huitwa mbolea za fosfeti (Phosphate Fertilizers), kundi hili lina mbolea kama MAP, TSP, DAP, Minjingu n.k

KUNDI LA PILI: MBOLEA ZA KUKUZIA:
Mbolea hizi huwekwa kipindi cha ukuaji wa mmea (vegetative growth) na hua na lengo la kuupa mmea ukuaji mzuri utakaopelekea kua na majani mazuri yatakayotengeneza chakula cha kutosha cha kwenye mmea.

Kitendo hichi cha mmea kutengeneza chakula chake huitwa Photosynthesis na hufanyikia kwenye majani. Kirutubisho kikuu katika kundi hili la mbolea ni Nitrogen (N). Baadhi ya mbolea zilizopo kwenye kundi hili ni pamoja na UREA, SA, CAN n.k.

Pia kwenye kundi hili zipo mbolea za maji zinazopigwa kwenye majani (foliar fertilizers) hujulikana pia kama booster.

KUNDI LA TATU: MBOLEA ZA KUZALISHA/KUKOMAZIA KITUNGU.
Hizi ni zile zinazowekwa kuusaidia  mmea kutengeneza kitunguu (bulb formation).  Kirutubisho kikuu hapa ni Potassium. Ili Kituunguu kiweze kujijenga vizuri na kua na ubora mzuri kinahitaji mbolea zenye kitutubisho cha Potassium. Mfano wa mbolea zenye virutubisho hichi ni Multi K, MOP (Muriate of Potash) n.k.

Hayo ndio makundi makuu ya mbolea, japokua mbolea hizo hujumuisha pia virutubisho vidogo (micro nutrients) ambavyo vinahitajika kwa udogo kwenye mimea, japokua zina kazi muhimu kwenye mimea.

MATUNZO YA BUSTANI YA VITUNGUU

PALIZI

Mmea wa kitunguu una mizizi mifupi, hii husababisha kutunguu kuathirika sana na ushindani na magugu. Mizizi mifupi ina maana huufanya kukosa uwezo wa kustahimili ushindani wa magugu.

Magugu yana uwezo mkubwa wa kufyonza virutubisho ardhini kuliko mimea ya mazao, na ndio maana magugu hukua kwa haraka kuliko mazao.  Hivyo inashauriwa katika shamba la vitunguu hakikisha unafanya palizi kwa wakati.

Idadi ya palizi inategemea na aina na wingi wa magugu wa eneo husika. Kwenye ameneo yenye magugu mengi, palizi hufika hadi 4, na kwa maeneo ambapo magugu sio tatizo palizi mbili zinatosha.

Kuna mbinu mbalimbali za kfuanya palizi kama matumizi ya dawa za kudhibiti magugu (herbicides), palizi ya mkono (hand weeding) na uwekaji wa matandazo (mulching).

UMWAGILIAJI
Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba.

Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua. Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu.

Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung’olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.

Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongokama sentimita 5.

Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU WA VITUNGUUMAGONJWA YA VITUNGUU     

A) Ukungu mweupe Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.Dalili za kugundua Ugonjwa huu     Utaona unga wa rangi ya zambarau katika majani.

Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kunyauka. Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.KuzuiaInashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu.

Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa mwingiTumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k.

Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.

B) UKUNGU WA KAHAWIA 
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.Dalili zake Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau.

Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,kidonda au mkwaruzo.

NAMNA YA KUZUIA
Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.

Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa kuchimba na jembe.Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.

C) UGONJWA WA KUOZA MIZIZI
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.Dalili Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka.

Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.KuzuiaTumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi mwingine.Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao.

Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu  mkubwa haujatokea.

WADUDU WAHARIBIFU 
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao hili:
VIROBOTO WA VITUNGUU Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.

Dalili za kugundua Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung’aa.

Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.Kuzuia Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35, Parathion nk.

Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako    liwe limekomaa. Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k.

Wadudu wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi.Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.CHAWA WEKUNDU. (THRIPS) Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu.

(Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu. Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka.

Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-Kuweka shamba katika hali ya usafi, Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu, Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.

SOTA (CUTWORMS)  Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao. Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka  shamba katika hali ya usafi.

UTITIRI WEKUNDU (RED SPIDER MITES) Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.Njia ya kudhibiti:      Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.      Kuteketeza masalia ya mazao      Kutumia mzunguko wa mazao

VIPEKECHA MAJANI (LEAF MINER) Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka.

Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.Njia ya dhibiti:Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na DursbanKuteketeza masalia ya mazaoKutumia mzunguko wa mazaoMAGUGU Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu.

Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen (Goal 2E).

Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali.  Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu  Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.

UVUNAJI WA VITUNGUU
Muda wa ukomaaji wa vitungu hutegemea aina ya vitunguu pamoja na hali ya hewa ya eneo husika. Aina za chotora  (hybrid) mara nyingi hukomaa mapema, huchukua miezi 3 hadi 5 baada ya kusia mbegu.  Aina za kawaida (OPV) na zile za kienyeji hazina ukomaaji unaofanana (do not mature uniformly), hukomaa kwa makundi makundi.

Pia mara nyingi hukomaa miezi 4 na kuendelea kuanzia kusia mbegu. Kama shamba lako unatumia umwagiliaji, basi umwagiliaji unapaswa kukoma siku 7 hadi 10 kabla ya kuvuna. Uvunaji unaanza pale majani ya vitunguu yanapoanza kukauka, kupoteza rangi na kujikunja.

Yale majani ya nje yanayofunika kitunguu unene wake unapungua. Hizo ndio dalili za kitunguu kua tayari kwa kuvunwa. Uvunaji wa mapema (early harvest) hupelekea vitunguu ambavyo havijakomaa vizuri, hivyo kusababisha kupoteza maji na  kusinyaa kwa vitunguu wakati wa ukaushaji wa vitunguu.

Pia uvunaji wa kuchelewa (late harvest) husabisha kitunguu kupoteza rangi yake, kuoza kwa yale maganda/majani yanayokua yamekifunika kitunguu chenyewe (onion bulb). Hivyo basi kitunguu kinapaswa kuvunwa kwa wakati sahihi ili kuepuka hasara inayoweza kutokana na kuwahi au kuchelewa katika uvunaji.

Wakati wa uvunaji, vitunguu hung’olewa toka ardhini, kisha kukatwa mizizi yake ili kuzuia ukuaji wa majani. Baada ya hapo ukaushaji wa vitunguu unaanza.



UKAUSHAJI WA VITUNGUU.

Baada ya kuvuna kitunguu, hatua inayofuata ni ukaushaji (curing) na hii inafanyikia palepale shambani. Kukausha kitunguu ni ule mchakato wa kukausha ile shingo ya kitunguu. Shingo ya kitunguu inapokauka inakifunga kitunguu, pia inaziba njia ambazo zinaweza kutumiwa na vijidudu kuingia ndani kuharibu kitungu.

Ukaushaji pia husaidia kupata kitunguu chenye ngozi iliyokauka na yenye rangi nzuri. Ngozi tunamaanisha lile ganda la nje lililofunika kitunguu.  Baada ya kung’olewa vitunguu shambani unavikusanya kwenye makundi makundi, kisha hayo makundi ya vitunguu unayafunika na majani makavu ili kuepuka kuchomkea na jua na kutengeneza mabaka ya kuchomwa na jua (Sunscald).

Muunguzo wa jua (sunscald) yaani kitunguu kinapopigwa na mionzi ya jua huua au huharibu lile ganda la nje na hivyo kupelekea kitunguu muundo usiofaa au kuvutia vijidudu vyenye kusababisha kitunguu kuoza. Viache vitunguu kwa muda wa wiki moja au mbili ili vikauke vizuri, kisha vipakie kwenye magunia kwa ajili ya kwenda kuhifahi au kwa ajili kupeleka sokoni.

UHIFADHI WA VITUNGUU (STORAGE)

Kitungu ndio zao lenye uwezo wa kuhifadhika kwa muda mrefu zaidi kuliko mazao yote ya mboga. Kitunguu baada ya kuvunwa bado kinakua ni kiumbe kinachoishi (living organism) ikimaanisha kinaenelea na michakato kama kupumua, kupoteza maji n.k Hivyo uhifadhi wake unahitaji umakini ili kuweza kukaa muda mrefu bila kuharibika.

Hii ni tofauti na mazao kama mahindi, maharage n.k, ambapo yakishakaushwa yanabaki na asimilia ndogo sana ya unyevunyevu, na unaweza kuyaweka kwenye pia au dramu na ukafunika na kuziba kabisa  bila kua na hata hewa, na mahidni yakaendelea kukaa salama kabisa. Ila kitunguu ni tofauti, kikikosa hewa kinaharibika. Mbinu na mifumo mizuri ya uhifahi wa kitunguu ni muhimu sana kwa maisha ya vitunguu.

Comments

Popular posts from this blog

KILIMO BORA CHA NYANYA NA SOKO LAKE

SOKO LA TIKITI MAJI NA KILIMO CHAKE

KILIMO BORA CHA VITUNGUU SAUMU NA SOKO LAKE